TUKIO la kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), kwa madai ya uchochezi, limeibua sura
mpya baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutajwa kuwa nyuma ya mkakati
huo, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Lema ambaye bado anaendelea kusota rumande siku ya tatu baada ya
kunyimwa dhamana, ameanza kufanyiwa vituko na Jeshi la Polisi baada ya
jana asubuhi mkewe kuzuiliwa asimpe mswaki wala chai.
Mbunge huyo alikamatwa kutokana na amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Magesa Mulongo, aliyedai kuwa aliwachochea wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu
Arusha kumzomea kiongozi huyo na kupopoa gari lake kwa mawe.
Hata hivyo, siku moja kabla ya kukamatwa Lema aliwaonesha waandishi wa
habari ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani aliyotumiwa na Mulongo
akimtishia kuwa atamfungulia kesi yoyote anayoitaka.
“Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonesha kuwa mimi ni
serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’
ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba 0752 960276 ambayo
Lema alidai ni ya Mulungo.
Pia nguvu kubwa iliyotumika kumkamata mbunge huyo usiku saa 5:30 kwa
kutumia askari na maofisa wa usalama kuzingira nyumba yake, imehojiwa na
baadhi ya wananchi, wakitilia shaka kuwa kuna siri ndani yake.
Madai ya Mulongo kuwa Lema alichochea wanafunzi hao yanakinzana na
ushahidi wa video unaoonesha kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya
ushawishi kuwasihi wasiandamane baada ya mwenzao, Elly Kago (22), kuuawa
na watu wasiojulikana jirani na chuo hicho.
Akizungumza na gazeti hili jana, mke wa Lema, Neema, alisema kuwa
alifika kituo cha polisi asubuhi akipeleka chai, lakini akaelezwa kuwa
haruhusiwi kumpelekea chai.
Alisema kuwa alipiga simu kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa ndipo
akaambiwa ampelekee na alipofika tena kituoni askari aliyekuwa zamu
alianza kupekua mfuko wa Neema kwa fimbo, kisha akaamuru Lema apewe, ila
anywe kwa dakika tatu.
Wakati anafungua chupa ya chai na kumimina kwenye kikombe, askari
alimweleza kuwa imebaki dakika moja, hatua iliyomuudhi Lema akidai ni
udhalilishaji, hivyo akashindwa kunywa.
Alipotaka kupewa mswaki, askari alikataa kuwa vifaa hivyo vinaweza kutumika kama silaha, hivyo haruhusiwi kupewa.
Tanzania Daima Jumapili lilizungumza na wanasheria kadhaa pamoja na
wanasiasa wabobezi kuhusu sakata hilo, ambapo baadhi walidai huo ni
mkakati wa CCM kutaka kuidhoofisha CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa
madiwani ujao kwenye kata nne.
“Kesho mnaweza kusikia Lema akifunguliwa kesi ya ajabu ya kutunga
halafu kwa kipindi hiki kampeni zikianza mahakama itakuwa ikiisikiliza
mfululizo ili asipate nafasi ya kushiriki kikamilifu.
“Huu mkakati si wa Mulongo peke yake bali ni mbinu za CCM zilizobakia
katika kuhakikisha wanaikamata Arusha. Lakini naona kama wanazidi
kujimaliza,” alisema mwanasiasa mmoja aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.
Mwanasiasa huyo kutoka mkoani Arusha aligusia pia mkanganyiko wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni kutangaza kata nne kurudia
uchaguzi na kuiacha moja ya Sombetini ambayo diwani wa CCM alihamia
CHADEMA.
“Ujue CCM wanafanya mambo bila kupima athari, Arusha ni mji wa kitalii
lakini kwa sasa unaogopeka kwa fujo za polisi na wanasiasa, hata kesho
utaona wakati Lema akipelekwa mahakamani.
“Hapa ni ngome ya CHADEMA hata kama Lema hayupo, sasa NEC wameibana
Sombetini kwa hofu kuwa kata zote zikienda CHADEMA watakuwa na madiwani
zaidi ya CCM, hivyo ishu ya meya kufufuka upya, ndiyo wakaamua kumtumia
Mulongo kufanya mchezo huu wa hatari,” alisema.
Alipopigiwa simu jana jioni na kuulizwa juu ya madai hayo, Mulongo
alizungumza kwa ukali akisema: “Wewe mhariri unaweza kunipigia simu
kuniuliza swali kana hilo?”
Aliendelea kufoka akisema: “Acheni kufanya kila kitu siasa, wewe ni
polisi kujua Lema kwanini akamatwe hivyo, niache mimi niko na wageni
wangu,” alisema na kukata simu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis
Stolla, alizungumzia suala la kukamatwa kwa Lema akisema kuwa nguvu
kubwa na utaratibu uliotumika kumkamata haukuwa wa busara.
Stolla alisema: “Kwa mujibu wa kifungu cha 58 na 59 vya sheria ya
ushahidi, Jeshi la Polisi au hata kama ni kwa amri ya mkuu wa mkoa ya
kukamata walipaswa kuchagua njia nyingine ya busara.
“Jeshi linaweza kuwa na mamlaka mapana ya kukamata au hata kama ni kwa
amri ya mahakama, busara huhitajika kutumika. Lema ni mbunge,
anafahamika na upatikanaji wake hauna utata, anapotuhumiwa kuhitajika
polisi busara inatumika kumwita au kumwandikia aende, si kumvizia kama
walivyofanya,” alisema.
Mwanasheria mwingine ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, alifafanua kuwa:
“Rais peke yake ndiye Amiri Jeshi. Uamiri jeshi wa rais haugawanyiki
mpaka kwa wakuu wa mikoa.
“Uamiri jeshi wa rais upo kikatiba, hauwezi kuwa wa wakuu wa mikoa au
wa wilaya. Ndiyo maana anayeamrisha polisi katika mkoa ni Kamanda wa
Polisi wa Mkoa, na wilayani anakuwapo ofisa anayeamrisha (OCD),”
alisema.
Aliongeza kuwa sheria zinaruhusu mkuu wa mkoa na wilaya kutoa amri ya
kukamata mtu kama hakuna askari lakini mtuhumiwa anapokamatwa sharti
aambiwe anakamatwa kwa kosa lipi na anayemkamata ajitambulishe.
Alisema kuwa siku ya tukio chuoni, polisi walikuwapo wakati Lema
akizungumza na wanafunzi na hawakuona kosa lolote kwake ndiyo maana
hawakumkamata, sasa iweje mkuu wa mkoa aje na amri.
Akizungumzia nguvu iliyotumika katika kumkamata Lema, Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Tanga, Aaron Mashuve,
aliliomba Jeshi la Polisi kuelekeza nguvu kama hizo katika kusaidia watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Alisema nguvu hiyo kama ingetumika wauaji hao wangekuwa wamekamatwa
badala ya polisi kupoteza muda kuhangaika na wanasiasa ambao wanaweza
hata kuitwa kituoni wakaenda kwa hiari yao.
Katika hatua nyingine, CHADEMA mkoani Arusha kimetangaza kumfungulia
mashtaka mkuu wa mkoa huo kwa tuhuma za kumtishia mbunge wao kwa ujumbe
wa maandishi, pia kumtaka athibitishe madai ya kuwa kifo cha mwanafunzi
kina uhusiano na masuala ya kisiasa.
Katibu wa mkoa wa chama hicho, Amani Golugwa, alisema taratibu za
kuyashughulikia masuala hayo yote mawili zinaendelea chini ya jopo la
wanasheria wa chama hicho.
Source: Tanzania Daima, 28 April, 2013
|